
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Adolf Mkenda, amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe kutoka Exim Bank ukiongozwa na ndugu Shani Kiswaga, Afisa Mkuu wa Fedha wa benki hiyo.

Kikao hicho kimefanyika leo, Aprili 27, 2026, jijini Dodoma, kikiwa na lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Benki ya Exim katika nyanja mbalimbali za maendeleo ya elimu.

Katika mazungumzo hayo, pande hizo mbili zimejadili fursa mbalimbali zikiwemo za ufadhili unaoweza kutolewa na benki hiyo kwa wanafunzi wa elimu ya juu hususan kupitia mpango wa Samia Scholarship kwa wanafunzi wanaosomea sayansi ya data (Data Science) na akili unde (Artificial Intelligence) na Sayansi shirikishi.

Aidha, ujumbe huo umepongeza Wizara kutekeleza mageuzi makubwa ya elimu nchini, hatua ambayo inawezesha kuandaa rasilimaliwatu yenye ujuzi.

Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Wizara hiyo,Mhe. Wanu Hafidh Ameir, pamoja na Naibu Katibu Mkuu, Prof. Daniel Mushi.


