Mwandishi wa Kitabu cha *Tangled Web* Euanice Urio ameiomba Serikali kusaidia katika mnyororo wa Sekta ya Uandishi wa Vitabu ili kuwezesha upatikanaji wa vitabu na kuhamasisha usomaji nchini
Akizungumza Agosti 02, 2024 Jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Kitabu chake hicho, Urio amesema kuwa changamoto kubwa katika sekta hiyo ni kuvipeleka sokoni kutokana na watanzania wengi kutokuwa na tabia ya usomaji wa vitabu.
Amesema kuwa ili kuondokana na changamoto hiyo ni kuhamasisha usomaji wa vitabu jambo ambalo ni gharama kubwa kwa waandishi kuweza kufanya hivyo na kuomba serikali isaidir katika upande huo.
"Ukweli usiopingika kwamba vitabu vinasaidia katika kutunza utamaduni na mila, historia ya nchi hivyo ni vyema serikali isaidie katika kuhakikisha kuna vitabu vilivyoandikwa na watanzania ili kupunguza usomaji wa vitabu vya nje ambavyo vimekuwa vikileta tamaduni zao ambazo wakati mwingine si sahihi kwetu" amesema Urio
Mwandishi huyo ameongeza kuwa watu wasipoandika vitabu itafika wakati nchi itapoteza historia na utamaduni kwa kuwa wananchi wanasoma vitabu vya nje.