Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amesema, Serikali inaendelea kuweka msisitizo suala la elimu, na katika Mwaka wa fedha 2024/25 imetenga Sh. bilioni 787 kwa ajili ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu.
Mhe. Majaliwa amesema hayo Agosti 27, 2024 akimwakilisha Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika sherehe za Miaka 50 ya Idara ya Ujenzi ya Chuo cha Sayansi na Teknolojia Karume (KIST) visiwani Zanzibar.
"Nawasihi Vijana wa Kitanzania kuchangamkia fursa za mafunzo katika fani za Sayansi na Teknolojia ambazo zinapewa kipaumbele na Serikali ili kuchochea maendeleo ya kijamii na Kiuchumi" Alisema Majaliwa.
Waziri Mkuu ameongeza kuwa ili kuongeza wigo Serikali inatekeleza mpango wa internship kwa Vijana, kwenda kwenye makampuni mbalimbali kupata ujuzi na utaalam, ambapo asilimia arobaini ya kipindi cha mazoezi yao ni nadharia na asilimia sitini ni kwa vitendo.
Ameipongeza Taasisi ya KIST kwa kusaidia kukuza sekta ya viwanda na ujenzi pamoja na miradi mikubwa inayotekelezwa Nchini ambayo inachochea uchumi.