Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda ameishukuru Serikali ya Canada kutangaza kuongeza ufadhili wa Dolla za Canada milioni 50 takriban shilingi Bilioni 95 za Tanzania kwa ajili ya kufadhili miradi ya Elimu Tanzania.
Prof. Mkenda ametoa shukrani hizo Julai 20, 2023 baada ya Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa na mwenye dhamana ya Shirika la Maendeleo ya Uchumi la Pasifiki wa Canada Mhe. Harjit S. Sajjan, kutangaza ongezeko hilo.
Prof. Mkenda amesema kuwa Dola milioni 25 zitatumika kuwezesha Wasichana kusoma na kukamilisha mzunguko wa Elimu na Dola milioni 25 za zitatumika kuendeleza mafunzo ya Amali kwa vijana kuwawezesha kupata ajira.
"Haya ni mafanikio ya Serikali kuendelea kujenga mahusiano mazuri na nchi mbalimbali na Rais wetu amekuwa akifanya kazi kubwa ya kuimarisha mahusiano hayo". Alisema Prof. Mkenda.
Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa na mwenye dhamana ya Shirika la Maendeleo ya Uchumi la Pasifiki la Canada Mhe. Harjit Sajjan amesema serikali ya nchi hiyo imekuwa Mshirika wa muda mrefu wa Tanzania katika sekta ya elimu na imefanikiwa kuboresha viwango na upatikanaji wa elimu katika Vyuo vya Ualimu na Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi katika kusaidia jitihada mbalimbali za serikali.
"Kwa kushirikiana na serikali tumewekeza katika mafunzo mathubuti kwa Walimu katika Vyuo 35 vya Ualimu" ambapo kwa miaka 14 Canada imetoa zaidi ya dollar za Canada milioni 250" Alibainisha Mhe. Sajjan.
Waziri huyo ameipongeza serikali ya Tanzania kwa kuruhusu wanafunzi waliokatisha masomo kwa sababu mbalimbali kurejea shuleni, ili kuwawezesha kupata maarifa na Ujuzi hivyo kushiriki katika uchumi.
Ameongeza kuwa uwekezaji katika Elimu hasa mtoto wa kike hubadilisha jamii, huimarisha uchumi na kuchangia jamii kuwa imara zaidi. Hivyo nchi hiyo itaendelea kushirikiana kuendeleza sekta ya Elimu.