Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani (NECTA) Dkt. Said Mohamed amesema kuwa kuanzia Mwaka huu hakutakuwa na maswali ya kuchagua katika mitihani ya Hisabati.
Akiwasilisha taarifa ya hali ya ufaulu na ujifunzaji wa wanafunzi Mei 30, 2024 Jijini Tanga Dkt. Mohamed amesema kuwa tayari mafunzo yameshatolewa kwa ajili ya kutekeleza hilo huku akihimiza ushirikiano kutoka kwa wadau mbalimbali.
Akizungumzia taarifa hiyo Katibu Mtendaji amesema Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ililiagiza Baraza hilo kufanya tathimini ya hali ya ufaulu na ujifunzaji wa wanafunzi katika masomo ya Hisabati, Bailojia, Fizikia na Ligha ya Kiingereza ili kuboresha ufundishaji na ujifunzaji
Akizungumza katika hafla hiyo Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema kuwa Serikali inaweka mikakati ya kuendelea kupima ubora wa elimu kitaifa nna Kimataifa.
Prof. Mkenda amesema kuwa bado kuna kazi kubwa ya kuboresha ubora wa elimu na kwamba suala muhimu ni kujipima kitaifa na kimataifa ili kuona elimu nchini ipo katika hali gani
Ameongeza kuwa mageuzi ya elimu yaliyofanyika yana maana pana na yameleta mfumo tofauti wa elimu nchini na kwamba ni muhimu kuwa na tathimini ili kuhakikisha elimu inayotolewa inakuwa bora
"Suala la kuwa na tathimini ya kweli ni muhimu, tunahitaji mfumo wa mtihani wenye weledi na uadilifu ili tuwe na uhakila wa tunachopata katika matokeo yake" amesema Waziri huyo
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo amesema kuwa taarifa hiyo inatoa picha halisi kuhusu ufundishaji na ujifunzaji katika shule za msingi na Sekondari ambapo mapendekezo yaliyotolewa yanaonesha dira ya nini cha kufanya kuhakikisha ufundishaji na tathimini katika ngazi ya shule za msingi na Sekondari
Katibu Mkuu huyo ameongeza kuwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inaendelea kushirikiana na wadau wa elimu katika kuhakikisha masuala ya ufundishaji, ujifunzaji na tathimini katika shule yanaimarishwa kwa lengo la kukuza umahiri wa wanafunzi katika masomo