Mhadhiri Mwandamizi Shule Kuu ya Elimu, Idara ya Saikolojia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dkt. Bernadetha Rushahu ameishauri jamii kupata huduma za ushauri na unasihi kutoka kwa Wataalam wa Saikolojia ili kukabiliana na changamoto ya Afya ya akili inayowakabili Watu wote ikiwemo wenye mahitaji Maalum.
Dkt. Bernadetha ametoa ushauri huo Septemba 18, 2024 jijini Arusha katika Kongamano sehemu ya Maadhimisho ya Miaka 30 ya Elimu Jumuishi, akiwasilisha mada kuhusu ushauri na unasihi, amesisitiza kuwa huduma hiyo inasaidia kuwezesha Wanafunzi wenye mahitaji maalum kuwa na ustawi bora na hivyo kuwa na maendeleo mazuri ya kitaaluma katika ngazi mbalimbali.
"Ushauri na unasihi ni muhimu katika jamii ya Kitanzania na kwa kila mmoja wetu, kwa sababu msongo wa mawazo na sonona vinamkumba mtu yeyote mwenye mahitaji Maalum na asiye na mahitaji Maalum" Alisema Dkt. Bernadetha.
Aidha Dkt. Bernadetha amewashauri pia Wadau mbalimbali kuwekeza kwenye eneo la ushauri na unasihi kuwezesha jamii kupata huduma bora na kwa urahisi ili kutunza afya wakati wote