
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, Aprili 11, 2025, amefungua rasmi Mkutano wa 35 wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo mkoani Morogoro, na kutoa wito kwa watumishi kuhakikisha wanasimamia kikamilifu utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo Toleo la 2023.
Amesema sera hiyo inalenga kuleta mageuzi ya kimfumo katika sekta ya elimu kwa kutoa maarifa na ujuzi unaohitajika katika karne ya 21, kupitia mikondo miwili ya elimu, Elimu ya Jumla na Elimu ya Amali, ili kumpa kila mwanafunzi fursa ya kuchagua njia inayomfaa kwa maisha na taaluma.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Charles Mahera, amesema wajumbe wa mkutano watajengewa uwezo kupitia mada mbalimbali, ikiwa ni pamoja na tathmini ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2024/2025 na mwelekeo wa bajeti ya mwaka 2025/2026.
Mkutano huo wa siku mbili umebeba kauli mbiu: “Elimu na Ujuzi kwa Maendeleo ya Taifa Letu – Tunatekeleza”.