Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda ameendelea na siku ya pili ya ziara ya kukagua utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo Mkoani Njombe.



Leo Septemba 21, 2024 Prof. Mkenda amezindua wa Kituo cha Afya Makoga katika jimbo la Wanging’ombe kilichojengwa na serikali kwa gharama ya zaidi ya milioni 500



Akizungumza na wananchi wa Makoga baada ya kuzindua Kituo hicho amewataka wananchi wanging’ombe kukitunza kituo hicho ambacho kinatoa huduma ya daraja la kwanza kutokana na kuwekewa vifaa tiba vya kisasa, madaktari na wauguzi.



“Uwekezaji huu mkubwa katika sekta ya afya umeleta maboresho makubwa ambayo yamefanya kuleta hata watu kutoka nje kufuata huduma za afya nchini, hivyo changamoto zinazofanyiwa kazi zisitukatishe tamaa ama kuona kama hakuna kinachofanyika” amesisitiza Waziri huyo



Mbunge wa Jimbo la Wanging’ombe ameishukuru Serukali ya Awamu ya Sita kwa kuwapatia Kituo hicho cha Afya ambacho miaka mitatu iliyopita hakukuwa na majengo hayo na wananchi walikuwa wakipata tabu ya kupata huduma.



Naye Mkuu wa Wilaya hiyo Zacharia Mwansasu amemweleza waziri kuwa wananchi wa Makoga walichangia nguvu kazi ambayo iliokoa fedha iliyotumika kujenga nyumba ya muuguzi. Ameongeza kuwa Serikali imetoa zaidi ya Shilingi Milioni 100 kwa ajili kuongeza vifaa tiba vya zahanati hiyo.



Mkazi wa Kata ya Makoa Lucy Chaula amemshukuru Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia Kituo cha Afya chenye wahudumu wanaojali wananchi pamoja na kuwapatia vifaa tiba vya kisasa hasa katika upande wa uzazi jambo ambalo limepunguza vifo.