Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Tume ya nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) imetangaza kutoa ufadhili wa masomo ya Chuo Kikuu nje ya nchi kwa asilimia miamoja kwa shahada za umahiri (MSc) katika fani za sayansi na teknolojia ya nyuklia.
Akizungumza na Waandishi wa Habari, Waziri katika Wizara hiyo Prof. Adolf Mkenda amesema Mwaka huu wa Fedha 2024/2025 Samia Scholarship Extended imetenga jumla ya Shilingi Bilioni 1.6 kuwezesha mpango huo.
Amesema Serikali inafanya uwekezaji kwenye la Sayansi na Teknolojia ya Nyuklia, ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii pamoja na kukidhi mahitaji makubwa ya huduma zitokanazo na Teknolojia ya nyuklia na upungufu wa wataalamu hapa nchini.
‘’Wizara imebaini ongezeko kubwa la matumizi haya hasa kwenye miradi mikubwa ya madini kama vile Urani, Madini Adimu na maeneo mengine ambayo yanahitaji nchi kuwa na wataalamu wa ndani na wabobezi kwelikweli’’ alisema Mkenda.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Mionzi Tanzania (TAEC) Prof. Najat Mohamed, amesema ufadhili unalenga eneo la Sayansi na Teknolojia ya Nyuklia katika; matibabu ya saratani, utafiti wa maji, hewa na mimea, unururishaji wa vifaa tiba, bidhaa za viwandani na mazao, nishati ya nyuklia na utafiti wa vinu vya nyuklia pamoja na uzalishaji wa dawa za mimea.
Amesema ufadhili huo utatolewa kwa waombaji wenye sifa katika Vyuo Vikuu vinavyotambuliwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kwenye nchi za Australia, Austria, Ubelgiji, Canada, China, Jamhuri ya Czech, Sweden, Ufaransa, India, Korea ya Kusini, Uturuki, Urusi, Finland, Uingereza na Marekani.