Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Adolf Mkenda leo Agosti 29, 2023 jijini Dar es Salaam amefungua Mkutano wa Taasisi za Kiislam na Wataalamu wa mitaala kujadili kuhusu mtaala wa somo la elimu ya dini ya kiislam katika Shule.

Akizungumza katika Mkutano huo Waziri Mkenda amesema kwa sasa Serikali iko katika kukamilisha mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 ili kutoa toleo la 2023 ambayo inatoa mwelekeo wa elimu nchini na kufanya mabadiliko ya mitaala inayo akisi Sera hiyo.

Katika kutekeleza kazi hiyo, Serikali imeshirikiana na wadau mbalimbali na kwamba mitaala imekamilika na iko katika Tovuti ya Taasisi ya Elimu Tanzania. Aidha amesisitiza kuwa ni muhimu wadau wote kuelewa na kuridhika na mitaala hiyo na kuongeza iwapo kuna uhitaji wa kujadiliana kwa ajili ya kuiboresha itafanyika hivyo.



"Tumekuja kuwasilikiza, kushauriana kuondoa mashaka yoyote yanayoweza kujitokeza hatufungi milango bado iko wazi ,"amesema Prof. Mkenda

Prof. Mkenda amemshukuru Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania na wadau wote wa taasisi hizo kwa kuona umuhimu wa kuandaa Mkutano huo muhimu.

Akitoa shukrani mara baada ya ufunguzi Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu BAKWATA Sheikh Khamis Said Mtaka amesema jambo la elimu linahitaji ushirikiano.

" Jambo hili la elimu ni letu sote na muhimu na ndio maana leo tumekutana na pia tunamshukuru Waziri Mkenda kwa ushirikiano na kuhakikisha tunafanikisha mkutano huu," amesema Mtaka

Mkutano huo umeshirikisha viongozi mbalimbali wa Wizara na wa Taasisi za kiislamu nchini akiwemo Mufti Mkuu wa Tanzania alieshiriki katika ufunguzi na Mufti Mkuu wa Zanzibar pamoja na wataalamu wa Mitaala. Mkutano huo unatarajiwa kutoa mapendekezo ya kuzingatiwa kuhusu Mtaala huo.