Serikali inaendelea kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika ujifunzaji na ufundishaji katika ngazi zote za elimu nchini kuanzia elimu ya awali hadi vyuo vikuu.



Hayo yameelezwa leo tarehe 16 Oktoba 2025 na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Hussein Mohamed Omar alipokutana na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Imagine World Tanzania Dkt. Jacqueline Mgumia katika Ofisi za Wizara jijini Dodoma



Dkt. Omar ameongeza kuwa Wizara tayari imeandaa Mkakati wa Matumizi ya Teknolojia za Kidijitali katika Elimu sambamba na miongozo ya kitaifa ya elimu kidigitali katika ngazi ya Elimu msingi, Elimu ya Ufundi na Elimu ya Juu ambapo amesisitiza kuwa kupitia mikakati hiyo Tanzania inaendelea kupiga hatua kubwa katika matumizi ya teknolojia kwenye sekta ya elimu nchini.



Kwa upande wake Dr. Mgumia ameishukuru Wizara kwa kuendelea kushirikiana na Taasisi hiyo ambayo inatekeleza mradi wa kuwezesha matumizi ya TEHAMA katika kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK) kwa wanafunzi wa darasa la kwanza na la pili kwa ngazi ya elimu msingi.

Amesema kupitia mradi huu unaotekelezwa katika mikoa 5 ya Tanzania Bara na 2 Zanzibar Shule 500 zitanufaika na mradi kwa kupatiwa vifaa (tablets) zenye programu za ujifunzaji ili kuongeza uelewa wa KKK. Mradi huu pia unatoa mafunzo kwa walimu na kufanya utafiti juu ya matokeo ya kufundisha kKK na matumizi ya TEHAMA katika madarasa ya awali.