Viongozi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia wamekutana kwa mara ingine na kufanya majadiliano na ujumbe wa Benki ya Dunia juu ya ushirikiano katika utekelezaji wa mageuzi makubwa ya elimu nchini.
Akizungumza katika kikao hicho Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema Serikali imekamilisha Rasimu ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 toleo la 2023 na maboresho ya mitaala ya elimu.
Prof. Mkenda amesema kuwa mageuzi hayo yatahitaji uwekezaji mkubwa ya miundombinu na vifaa vya kufundishia na kujifunzia ambapo tayari Serikali imeanza kuweka mikakati mbalimbali ya upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya utekelezaji huo.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof. Carolyne Nombo amesema kuwa pamoja na mambo mengine mageuzi yamezingatia pia suala la uandaaji wa walimu, masuala ya TEHAMA katika Ufundishaji na ujifunzaji na kwamba hata sasa Serikali inaendelea na Mafunzo endelevu kwa walimu kazini pamoja na kuimarisha vituo vya walimu(TRC's).
Mkurugenzi Uendelezaji Rasilimali Watu Ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika kutoka Benki ya Dunia Daniel Dulitzky amesema benki hiyo ipo tayari kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza mageuzi hayo mbali mbali za elimu.