Chama cha Skauti Tanzania kimetakiwa kuendelea kufuata na kuheshimu Katiba ambayo ndio Dira ya Chama hicho ili kuepusha migogoro.

Rai hiyo imetolewa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda Jijini Dar es Salaam Julai 28, 2023 wakati akizungumza katika halfa ya kuwaaga na kuwakabidhi bendera Skauti wanaokwenda Korea kushiriki Jamboree.

Prof. Mkenda amesema kuwa mgogoro uliokuwepo awali ulikuwa mgumu na kwamba ulisababishwa na kutokufuata katiba au tafsiri tofauti za katiba hiyo, hivyo ni vema wote mkawa na uelewa sawa.

"Nafurahi leo nimekuja kuna utulivu katika na mmesimama imara" amesema Prof. Mkenda.



Akizungumzia safari ya Skauti hao amewataka kuwa mabalozi wazuri kwa kuwa na nidhamu ya hali ya juu na kuwa mfano mzuri kwa kufuata taratibu na Sheria za Kongamano.

" Nitafurahi kusikia mmekwenda kule mkiwa na nidhamu nzuri na kushiriki kikamilifu katika kazi na mkawe mabalozi wazuri wa nchi yetu katika malezi" amesisitiza Waziri Mkenda.

Profesa Mkenda pia amewataka Maskauti hao na viongozi wanaokwenda Korea pia kuwa mabalozi wa Utalii na kuwakadhi bidhaa mbalimbali za kutangaza nchi.

Aidha,amewapongeza wadau mbalimbali walioshirikiana na Skauti katika kuwezesha safari hiyo wakiwemo Bodi ya Utalii na Assemble Insuarance.

Amesema kuwa serikali itahakikisha inaendeleza Skauti hasa katika Shule kwani inawawezesha vijan kujifunza namna ya kuwa mtu bora zaidi.

Naye Kiongozi wa Msafara huo Kamishna Mkuu mambo ya Nje Chama cha Skauti Fredrick Nguma amesema Jamboree ni tukio kubwa la kiskauti linalofanyika katika mfumo wa kambi ya nje na kuwakutanisha vijana wa skauti kutoka Duniani kote kubadilishana uzoefu na taarifa juu ya masuala ya utamaduni, teknolojia na mazingira.