Mwakilishi wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo Mhe. Mabula Magangila, amesema kuwa kuwaelimisha na kuwahamasisha watoto wa kike katika masomo ya sayansi ni hatua muhimu ya kimkakati, itakayowawezesha kufanya vizuri zaidi na kuchochea maendeleo ya Taifa.



Mhe. Magangila ameeleza hayo Februari 11, 2026 jijini Dodoma katika Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake na Wasichana katika, Sayansi, amesisitiza kuwa Sayansi ndio suluhisho la changamoto mbalimbali za kijamii na kiuchumi.



"Tuendelee kuhamisisha watoto wa kike kusoma sayansi na Bunge litaendelea kutunga sheria bora ili kuhakikisha mtoto wa kike anaendelea kupata elimu bora ikiwemo katika nyanja za Sayansi," amesema Mhe. Magangila



Amesema Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo inajivunia jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambayo kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeendelea kuimarisha Sekta ya elimu na Sayansi nchini hatua inayiwezesha Watanzania kukabiliana kwa ufanisi zaidi na changamoto za kijamii na kiuchumi zinazoikabili dunia ya sasa.