
Serikali ya Tanzania inasisitiza umuhimu wa kuwekeza katika ujuzi wa usalama wa mtandao ili kulinda uchumi wa taifa unaozidi kukua kidijitali.

Kauli hiyo imetolewa Aprili 11, 2026 jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir akizungumza katika fainali za Cyber Premier League (CPL), amesema kuwa vijana nchini wana nafasi kubwa ya kuwa walinzi wa mifumo ya kidijitali.

Amesema mashindano hayo ni jukwaa muhimu la kuibua na kukuza vipaji vya vijana katika eneo la usalama wa mtandao.

Mhe. Ameir, amepongeza mashindano hayo, akieleza kuwa yanaunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita za kujenga kizazi chenye ujuzi wa kutumia teknolojia kwa usalama na tija.

Ameongeza kuwa, uongozi wa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan umeweka mikakati mbalimbali ikiwemo Mkakati wa Taifa wa Elimu ya Kidijitali (2024/2025–2029/2030) pamoja na Mkakati wa Uchumi wa Kidijitali 2025, inayolenga kukuza matumizi salama ya teknolojia na kuandaa wataalamu mahiri.

Amesisitiza kuwa mafanikio ya uchumi wa kidijitali yanategemea uwepo wa wataalamu wenye uwezo wa kulinda mifumo ya sekta muhimu kama benki, afya na mawasiliano.

Kwa upande mwingine, Amesema Serikali inaendelea kutoa ufadhili kupitia mpango wa Samia Extended Scholarship kwa wanafunzi wanaofaulu katika masomo ya sayansi na hisabati, ili kuwaandaa wataalamu wa fani za kidijitali.


