Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Prof. Makenya Maboko, ameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa juhudi zinazoendelea za utekelezaji wa mageuzi ya elimu yanayolenga kuimarisha ubora wa elimu na kuchochea maendeleo ya taifa.



Prof. Maboko ametoa pongezi hizo Machi 6, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Bodi mpya kwa kipindi cha mwaka 2026 - 2029, ambapo amesema kuwa katika kipindi cha siku 100 za uongozi wa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, sekta ya elimu imepiga hatua kubwa kupitia utekelezaji wa mipango na mikakati mbalimbali ya maendeleo ya elimu.



“Katika kipindi hiki, tumeshuhudia kazi nyingi zimefanyika ikiwemo uzinduzi wa Mkakati wa Kisayansi wa (KKK) pamoja na uzinduzi wa Mpango wa Ushirikiano kati ya Taasisi za Elimu na Waajiri,” alisema Prof. Maboko.



Aidha, amesisitiza kuwa TCU itaendelea kushirikiana kwa karibu na wadau mbalimbali wa elimu katika kutekeleza majukumu kwa weledi, uwajibikaji na uzalendo na kwamba ipo tayari kupokea na kutekeleza maelekezo ya Serikali ili kuendeleza na kuimarisha sekta ya elimu nchini.