Mhe. Prof. Adolf Mkenda (MB), Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia ameshiriki Mkutano wa 22 wa Mawaziri wa Elimu wa Nchi za Jumuiya ya Madola unaofanyika katika Makao Makuu ya Jumuiya hiyo, Marlborougj House, London, Uingereza kuanzia tarehe 16 hadi 17 Mei 2024.
Mkutano huo unakutanisha Mawaziri wa Elimu, Taasisi za Jumuiya ya Madola, Mashirika ya Kimataifa kama UNESCO na Benki ya Dunia pamoja na wadau wengine wa elimu, kujadili namna nchi wanachama zinavyoweza kuweka mikakati stahimilivu itayoweza kuifanya elimu iwe endelevu katika kipindi cha majanga kama UVIKO-19; kuongeza fursa na usawa katika kuelimisha watu katika jamii; na kutumia teknolojia mpya kama vile akili bandi na teknolojia za kidijitali katika kurahisisha utoaji na upatikanaji wa elimu katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola.
Kutokana na JYM kuwa na uwakilishi wa nchi kubwa na visiwa vidogo, Sekretarieti ya Jumuiya hiyo inatumika kama jukwaa la kubadilishana uzoefu, kupeana maarifa na misaada ya kiteknolojia na kiufundi katika kutimiza azma hiyo. Pamoja na masuala mengine, Mkutano huo unatoa fursa kwa Mawaziri kujadili mchango wa ubunifu (innovation) katika kuimarisha sekta ya elimu.
Kipaumbele cha Serikali katika Mkutano huo ni kuona namna Tanzania inavyoweza kunufaika na ushirikiano na nchi wanachama wa Junuiya hiyo katika kuimarisha utoaji wa elimu ya ufundi na ujuzi mbalimbali utakaosaidia kupanua soko la ajira kwa vijana sambamba na mfumo rasmi wa elimu.
Pichani ni Mhe. Waziri Mkenda akiwa pamoja na Mhe. Patricia Scotland, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola.