Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema serikali itaendelea na kazi kubwa ya kuboresha miundombinu na kuweka vifaa vya kufundishia na kujifunzia katika Shule.
Prof. Mkenda amesema hayo Juni 25, 2024 Jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya utoaji wa Tuzo kwa walimu walioshinda shindano la pili la stadi za kufundisha somo la Kiingereza kwa Shule za Msingi kwa Tanzania Bara.
Mkenda amesema kuwa ni muhimu kuwekeza katika miundombinu, vifaa na walimu katika kuhakikisha elimu inayotolewa kwa watoto wa Kitanzania inakuwa bora na kuwawezesha kuwa na stadi, maarifa na umahiri.
Aidha, amewapongeza walimu wote nchi kwa kujitoa kwa juhudi kubwa kufundisha watoto ambapo wengine wamekuwa wakitumia mbinu na zana zinazoandaliwa kutokana na vifaa vinavyopatikana katika mazingira waliyopo.