Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Wilson Mahera amesema katumieni Maarifa, Ujuzi na Ubunifu wote mlioupata katika Mafunzo haya kwa kutekeleza kwa vitendo katika kuwawezesha wadau wote wa Elimu waliopo kwenye maeneo yanayowazunguka ili utekelezaji wa Mtaala wa Elimu ya Amali Sekondari ulete Tija kwa Taifa

Ameyasema hayo disemba 02 2024, Jiiini Arusha wakati akifunga Mafunzo ya Wathibiti Ubora wa Shule 340 kwenye mafunzo endelevu kazini ya namna ya kutathimi shule za Sekondari zenye mkondo wa Amali 

Dkt Mahera amesema Mageuzi haya ya kielimu yanalenga kutoa Elimu bora kwa kuandaa wahitimu wenye Ujuzi, Maarifa, Stadi, Ubunifu na mwelekeo chanya na wanaoweza kujiajiri au kuajiriwa na hivyo kukidhi mahitaji ya soko la ajira lililopo nchini, Kikanda na Kimataifa

“Ninyi Maafisa Uthibiti Ubora wa Shule mna jukumu kubwa la kufanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa mitaala iliyoboreshwa katika asasi zote za elimu nchini ili kujiridhisha kama utekelezaji unafanyika kama ilivyokusudiwa na Serikali” alisema naibu Katibu Mkuu huyo

mafunzo haya yamelenga kuwawezesha Wathibiti Ubora wa Shule kujengewa uwezo katika eneo hili la Amali kwa lengo la kuwawezesha kufanya Tathmini ya Elimu ya Amali kwa ufanisi ili kukidhi mahitaji ya mabadiliko na mageuzi haya makubwa yaliyofanywa na Serikali katika Mtaala wa Elimu ya Sekondari hasa katika eneo la Amali

Aidha Dkt Mahera amesema ni matumaini yangu kuwa mtakwenda kuyatekeleza kwa ufanisi yote mliyowezeshwa na wataalam hawa, mkaambukize ujuzi mlioupata kwa Wathibiti Ubora wa Shule wenzenu, Maafisa Elimu wa Wilaya na Kata, watendaji wa serikali, vyama vya siasa, walimu, wanafunzi na jamii kwa ujumla

Kwa upande wake Kamishna wa Elimu Dkt Lyabwene Mtahabwa amesema katika kazi ya Uthibiti Ubora wa shule ili ufanikiwe lenga kujenga mazingira salama, rafiki na kuleta chachu kwa walimu, wanafunzi na jamii katika kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji.