Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa kulihutubia Bunge aliweka bayana dhamira ya serikali yake ya kufanya mapitio ya Sera ya Elimu ya mwaka 2014 na kufanya mabadiliko ya Mitaala iliyopo ili ielekezwe kwenye kutoa elimu ujuzi kulingana na mahitaji ya soko kitaifa, kikanda na kimataifa.
Ndani ya miaka miwili ya uongozi wa Rais Samia kumeshuhudiwa maboresho makubwa katika sekta ya elimu na utekelezaji wa kazi kulingana azma yake ya kuhakikisha elimu inakuwa ni kichocheo kikubwa cha maendeleo kwa kutoa wahitimu wenye ujuzi na stadi.
Akizungumza katika nyakati mbalimbali, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda alisema Wizara imeendelea kutekeleza mikakati ya kukuza na kuongeza fursa za upatikanaji wa elimu katika ngazi zote za elimu na kuhamasisha na kuendeleza teknolojia na ubunifu wa ndani ikiwa ni pamoja kuzibiasharisha.
Alisema Wizara imeweza kutekeleza kazi kubwa ya kufanya mabadiliko ya mitaala ya elimu na Mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 na kuwa rasimu za Mitaala hiyo ya elimu msingi na sera muda si mrefu itatolewa kwa wananchi kwa ajili ya kupata maoni ya mwisho.
“ Pia mapitio ya mitaala kwa ngazi ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi pamoja na Elimu ya Juu yanaendelea kwa lengo la kuhakikisha elimu inayotolewa ni bora na inawajengea wahitimu kuwa na ujuzi na maarifa yatakayowapatia stadi zitakazo wawezesha kushiriki katika shughuli za kiuchumi kitaifa na kimataifa”
Kwa upande wa Elimu ya Juu, Profesa Mkenda alisema Serikali imeendelea kuhakikisha wanafunzi wa Elimu ya Juu wanasoma katika mazingira rafiki na wezeshi. Serikali ya Awamu ya Sita imelenga kukuza uchumi na kuboresha huduma za kijamii kama elimu kwa uwiano sawia katika mikoa na maeneo yote.
Alisema serikali ilitafuta na kupata mkopo wa Sh bilioni 972 wenye riba nafuu kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya kutekeleza Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), lengo la kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika vyuo vikuu pamoja na kuongeza kampasi zaidi.
Kupitia mradi wa HEET, zitajengwa Kampasi 14 mpya za vyuo vikuu katika mikoa ya ambayo haina vyuo vikuu ikiwemo ya Kigoma, Ruvuma, Singida, Mwanza, Kagera, Tanga, Buyu Zanzibar , Tabora, Manyara, Simiyu, Shinyanga, Lindi, Rukwa, na Katavi.
Kupitia mradi huo pia yatajengwa mabweni 34; vyumba vya mihadhara na madarasa 130; kumbi za mikutano ya kisayansi 23; maabara/karakana za kufundishia 108; miundombinu ya shambani na vituo atamizi 10 hatua ambayo itasaidia kuongeza idadi ya wanafunzi wanaosoma programu za kipaumbele Sayansi, Teknolojia, uhandisi na Hesabu (STEM) kutoka wanafunzi 40, 0000 kwa mwaka 2020 hadi kufikia 106,000 mwaka 2026.
Pia utaboresha mitaala ya programu za kipaumbele cha Taifa kwa kuhuisha na kuandaa mitaala mipya zaidi ya 290, kusomesha Wahadhiri 387 na wahadhiri 3500 wanatarajiwa kupata mafunzo kwa vitendo viwandani ifikapo mwaka 2026.
Kwa upande wa kuongeza fursa za elimu bajeti ya fedha za mikopo ya elimu ya juu imeongezeka kutoka Sh bilioni 570 katika mwaka wa fedha 2021/22 hadi kufikia bilioni 654 mwaka 2022/23 hivyo kufanya jumla ya wanufaika kuongezeka kutoka wanafunzi 177,892 mwaka 2020/21 hadi wanafunzi 202,016, kwa mwaka 2022/23. Alisema pia Serikali iliondoa TOZO ya asilimia 6 ya kulinda thamani ya fedha katika urejeshaji wa mkopo na tozo ya adhabu ya asilimia 10 ya mkopo wanatozwa kwa wanufaika.
Pia kumekuwa na ongezeko la udahili wa wanafunzi wa elimu ya juu kutoka 87,934 mwaka 2020/21 hadi 106,620 mwaka 2021/22, na mwaka 2022/2023 udahili umefikia 113, 383.
“ mwaka 2022/23 Serikali pia imeanzisha mpango wa kusomesha wanafunzi wenye ufaulu wa juu wa Kidato cha Sita katika masomo ya Sayansi ambayo ni moja ya kipaumbele cha Taifa kupitia Mpango wa Samia Skolashipu na jumla ya shilingi bilioni 3 zimetengwa ambapo wanafunzi 640 wamenufaika na ufadhili huu wamedahuliwa katika vyuo mbalimbali nchini”
Profesa Mkenda alisema katika kuongeza fursa za mafunzo ya ufundi stadi, Serikali imetumia kiasi cha Sh bilioni 30.84 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Vyuo vya Ufundi Stadi vya Wilaya 25 kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO 19.
katika kutekeleza azma ya Serikali ya kuwa na chuo cha VETA cha wilaya katika kila Wilaya na katika kila Mkoa, imetenga Shilingi bilioni 100 kwa ajili ya kuwezesha kuanza ujenzi wa Vyuo 64 vya VETA ngazi ya Wilaya katika Wilaya ambazo hazina vyuo vya ngazi hiyo pamoja na kuanza kwa ujenzi wa Chuo cha VETA ngazi ya Mkoa katika Mkoa wa Songwe ambao hauna chuo katika ngazi hiyo.
Serikali pia inakamilisha ujenzi wa Chuo kipya cha kisasa cha cha Ufundi Dodoma kwa gharama ya zaidi ya shilingi Bilioni 17 kwa awamu ya kwanza ambapo kikikamilika kitakachokuwa na uwezo wa kudahili Wanafunzi 15,000 kwa mara moja. Chuo hiki kikikamilika kabisa kitakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi zaidi ya 3000.
Katika kuboresha Mazingira ya kujifunzia na kufundishia katika vyuo vya ualimu, Serikali imetumia shilingi bilioni 100 kwa ajili ya ujenzi, upanuzi na ukarabati wa vyuo vinne na kukarabati 27 hatua ambayo itaongeza udahili kutoka 17,000 hadi kufikia zaidi ya 22,000. Katika kuimarisha matumizi ya TEHAMA kwenye ufundishaji na ujifunzaji, Serikali imegawa Vishwambi kwa Walimu wote wa shule za umma Tanzania Bara na Zanzibar. Vile vile wakufunzi wote wa vyuo vya ualimu na VETA, Vyuo vya Maendeleo vya Wananchi (FDCs) na wathibiti Ubora wa Shule wamepatiwa vishkwambi hivyo ili kurahisisha ufundishaji na ujifunzaji. Jumla ya vishkwambi 285,451 vimegawiwa kwa makundi hayo.
Alisema pia serikali imejenga Shule ya Mfano ya Sekondari iliyopo Iyumbu jijini Dodoma kwa gharama ya shilingi zaidi ya bilioni 17 ambayo ikikamilika itakuwa na uwezo wa kuchukua Wanafunzi 1000 kwa wakati mmoja, Ujenzi wa Shule ya Msingi ya Mfano jumuishi Lukuledi kwa gharama ya zaidi ya bilioni moja itakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 320 kwa wakati mmoja na Ujenzi wa Shule ya Mfano jumuishi ya Awali, Msingi, Sekondari ya Mbuye iliyopo Chato kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni nne itakuwa na uwezo wa kuchukua Wanafunzi 680 kwa wakati mmoja lengo ni kuongeza fursa za upatikanaji wa elimu iliyo bora katika mazingira salama kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Alisema katika sekta ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu, tumeona namna Serikali ilivyofanikiwa kuibua Wabunifu wapatao 1,581 ambapo kati yao 153 wametambuliwa na 27 wameendelezwa na 9 kati yao wamefikia katika hatua ya kubiasharisha utafiti zao. Lakini katika kipindi hiki cha miaka miwili tumeona Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu yakipelekwa mpaka katika ngazi ya wilaya, lengo likiwa ni kuwapata wabunifu waliopo chini na kukuza ubunifu na Teknolojia zinazozalishwa.
Kupitia Mradi wa SEQUIP Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Raisi Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imejenga Shule 232 za Sekondari na Shule za Sekondari za wasichana za Sayansi katika mikao 10 ambapo lengo ni kujenga shule hizo katika kila mkoa ili kusogeza fursa za watoto kusoma sayansi karibu na mazingira yao.
“ Moja ya eneo kubwa la kujivunia ni Serikali kutoa fursa ya wanafunzi walioacha shule kwa sababu mbalimbali ikiwemo ujauzito kurejea shule ambapo hadi kufikia January, 2023 wanafunzi zaidi ya 3,300 wamerejea shule, hili pia limetokea katika kipindi cha miaka miwili ya Mhe Samia.”
Alisema Serikali ya awamu ya sita imeazimia na inahakikisha kila mtoto bila kujali hali ya ulemavu anapata fursa ya kupata elimu bila vikwazo, Serikali imenunua vifaa wezeshi na malipo ya bima za afya kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum kwa gharama ya Sh milioni 664.
Pia imenunua vishikwambi (Tablets) 330 kwa ajili ya wanafunzi viziwi vyenye gharama ya Sh milioni 134 kwa ajili ya shule 15 za msingi zinazopokea wanafunzi viziwi. imenunua vitimwendo 1,334 vyenye thamani ya Shilingi milioni 191 kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu wa viungo waliobainika kuwa na uhitaji katika shule za msingi na sekondari.
Ubora wa elimu unaendana na uwepo wa mifumo sahihi, nguvu kazi na vitendea kazi kwa ajili ya usimamizi na uthibiti ubora wa Elimu. Katika pindi cha miaka miwili ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali imenunua na kusambaza magari 38 kwa ajili ya ofisi za uthibiti ubora wa shule kwa lengo la kuimarisha uthibiti wa elimu nchini. Samabamba na hilo, Serikali imetoa jumla ya Shilingi bilioni 2.6 kwa kuimarisha ufuatiliaji wa ufundishaji shuleni na kuwawezesha Maafisa Uthibiti Ubora wa Shule kutoa ushauri kwa lengo la kuboresha elimu.
“Wizara inajivunia na kushukuru maono na uongozi mahiri wa Mheshimiwa Rais Samia na kumshukuru kwa kuendelea kutoa kipaumbele katika sekta ya Elimu.