
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Daniel Mushi, Oktoba 15, 2025 jijini Dodoma ameshiriki Mkutano wa Tatu wa kitaifa wa Kamati ya Makatibu Wakuu kuhusu Mradi wa Uongezaji Thamani na kukuza Masoko ya Ndani na Nje ya Nchi (MARKUP II) ya mazao ya kimkakati.

Lengo kuu la Mradi huo ni kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ikiwamo Tanzania kwa kuongeza thamani katika bidhaa za kimkakati pamoja na kukuza mauzo ya bidhaa husika ndani na nje ya Jumuiya hiyo huku msisitizo ukiwekwa kwenye mauzo katika nchi za Umoja wa Ulaya (EU).

Akizungunza katika Mkutano huo Prof. Mushi amesema Serikali ya Tanzania imejizatiti kupitia Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo la 2023 kuhakikisha inazalisha wataalamu wenye ujuzi wa ngazi mbalimbali na katika sekta mbalimbali ikiwemo za kilimo na mifugo.

"nikitolea mfano sekta ya uzalishaji mazao ya ngozi Wizara ya Elimu imewekeza miundombinu ya kisasa katika Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT) Kampasi ya Mwanza Kupitia Mradi wa Afrika Mashariki wa Kujenga Ujuzi kwa Mlingano wa Kikanda (EASTRIP) ili kuimarisha mafunzo na kuwezesha uzalishaji wa bidhaa za ngozi kwa viwango bora na kwa wingi kwa ajili ya soko la ndani na nje". Amesema Prof. Mushi.


