Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema mageuzi ya Elimu yanayotekelezwa Nchini yanalenga kupata wahitimu mahiri wenye ujuzi ili waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za  ujenzi wa uchumi.

Waziri Mkenda ameeleza hayo Agosti 30, 2024 Mkoani Pwani  katika Mkutano wa waliokuwa Viongozi wa Serikali ya Wanafunzi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DARUSO) akimwakilisha Rais Mstaafuu wa Tanzania DKt. Jakaya Kikwete.

 Mkenda  amesisitiza kuwa  mageuzi ya Mitaala ambayo yamefanyika mpaka ngazi ya Vyuo vya ualimu yanalenga kuongeza ubora wa elimu.

"Dunia yote hii ni uwanja wa ajira kwa kila mtu, hivyo pamoja na kuwafundisha, tunapaswa kuwapatia ujuzi Vijana wetu ili waweze kujiamini na kutumia fursa mbalimbali za ajira ndani na nje ya Tanzania" Alisema Prof. Mkenda.

Nae Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya Mkutano huo Bw. Deo Mbasa amesema Viongozi hao ambao ni Alumni wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam wamekutana  kutathamini mchango wa Serikali za Wanafunzi katika kuandaa Viongozi wa kesho.