Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo amesema Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, Toleo la 2023, imezingatia na kusisitiza matumizi ya teknolojia za kidijitali katika sekta ya elimu ili kurahisisha ujifunzaji na ufundishaji.



Aidha, pamoja na masuala mengine, amesisitiza dhamira ya Serikali katika kujenga uwezo na kuzalisha walimu mahiri kwenye matumizi ya teknolojia za kidijitali.



Prof. Nombo ameeleza hayo Januari 08, 2025 jijini Dodoma akizungumza na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Ubelgiji-ENABEL, Bw. Koenaraad Goekint, juu ya mradi unaotekelezwa na Shirika hilo nchini kwa lengo la kujenga uwezo na kuimarisha mazingira ya utoaji wa elimu kidigitali.



‘’Utoaji wa elimu kidijitali ni kipaumbele chetu, vipaumbele vyenu na mradi mnaotekeleza unasadifu malengo yetu yanayodhamiria kuwezesha ujuzi wa teknolojia za kidijitali kwa vijana na walimu’’ alisema Prof. Nombo.



Goekint amesema Shirika hilo limejitolea, pamoja na maeneo mengine, kuimarisha utoaji wa elimu jumuishi kama nyenzo ya kufikia uchumi endelevu.

Aidha, Goekint alifafanua kwamba mradi wa elimu ya ubunifu wa dijitali utaimarisha uwezo wa kufundisha stadi za kidigitali.



Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu, Prof. Ladslaus Mnyone amesema kuwa teknolojia za kidijitali ni nyenzo muhimu katika kuharakisha mageuzi kwenye sekta ya elimu na sekta nyingine, hivyo kupitia utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa masuala hayo, Serikali imedhamiria kuimarisha mazingira ya kujifunzia na kufundishia stadi za kidijitali hususan kwa watoto na vijana.