
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidh Ameir, amewataka wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kutumia fursa ya mikopo ya elimu ya juu inayotolewa na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB), ili waweze kujiendeleza kielimu na hatimaye kuwa rasilimali muhimu kwa jamii na taifa kwa ujumla.

Aidha, Mhe. Naibu Waziri amewapongeza wahitimu wote kwa kufanikisha kukamilisha masomo yao na kuwataka kuwa mfano bora kwa jamii, akisisitiza kuwa elimu ya juu ni nguzo muhimu ya maendeleo ya taifa na muungano kwa ujumla.

Mhe. Wanu alitoa salamu hizo kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolph Mkenda, wakati wa mahafali ya 21 ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) yaliyofanyika Disemba 20, 2025, katika Ukumbi wa Dkt. Ali Mohammed Shein uliopo Kampasi Kuu ya Tunguu, Zanzibar. Amempongeza Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi, ambaye pia ni Mkuu wa SUZA, kwa kuendelea kukisimamia chuo hicho kitaaluma na kimaadili licha ya majukumu yake mengi ya kitaifa.


