Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amekemea vikali udanyanyifu wa mitihani unaofanywa na baadhi ya watumishi wa Serikali wasio waaminifu na kuwataka Wakuu wa shule kutojiingiza katika udanganyifu huo.
Waziri Mkenda ameyasema hayo Jijini Dodoma wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 17 wa Umoja wa Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (TAHOSA) ambapo amesema kwa kufanya hivyo ni kuandaa taifa ambalo litashindwa kufanya kazi kwa ufanisi.
Amesema mitihani imekuwa ikienda vizuri kwenye Baraza la Mitihani la Tanzania isipokuwa inapokwenda shuleni wamekuwepo watu wachache sana ambao wanajihusisha na udanganyifu na kwamba Serikali haitavumilia udanganyifu huo.
“Anayeleta udanganyifu kwenye mitihani tutamkamata, walimu hakikisheni mnakataa kujiingiza katika udanganyifu huo na kuwa makini zaidi kwenye masuala ya mtihani,” amesisitiza Waziri Mkenda.
Na kuongeza kuwa "Kwa sasa kuna kesi zinaendelea kwa wale ambao walituhumiwa kwa kuvujisha mitihani na nawaahidi pindi hukumu zao zitakopotolewa na Mahakama, tutaweka majina yao hadharani ili kila mmoja asijaribu kujihusisha na udanganyifu huo."
Akizungumzia suala la malezi shuleni Waziri Mkenda amewataka walimu kufuata Mwongozo wa Malezi, Unasihi na Ulinzi wa Mtoto katika Shule za Msingi, Sekondari na Vyuo vya Ualimu wa 2020 na kwamba kama kuna changamoto zibainishwe.
“Tushirikiane kufanya ulinzi wa watoto, hakikisheni shuleni hawalali watoto wawili kitanda kimoja na kama kuna changamoto ya vyoo toeni taarifa kwa Mkurugenzi kuhusu changamoto hizo, lengo ni kuhakikisha kunakuwepo na mazingira salama ya utoaji elimu na kuwalinda watoto,” amesisitiza Waziri Mkenda.
Amewataka Walimu kuangalia maudhui ya vitabu vinavyoingia shuleni ili visiharibu wanafunzi lakini pia kutumia Skauti na Viongozi wa dini katika kuendeleza malezi mazuri ya watoto shuleni.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Dkt. Charles Msonde amewataka Wakuu wa Shule kufuatilia utendaji wa walimu shuleni ili kuondoa alama F kwenye masomo wanayofundisha.
“Naendelea kusisitiza kufuatilia utendaji wa walimu, lakini pia wanafunzi wanapoingia shuleni tuanze na kuhakikisha wanakuwa vizuri katika lugha, wanapoilewa na kuweza kuiandika inakuwa rahisi kwao kuelewa masomo,” amesisitiza Dkt. Msonde.
Kwa upande wake Rais wa Umoja wa Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (TAHOSA), Frank Mahenge ameishukuru Serikali kwa namna inavyoshirikiana na Umoja huo na kuiomba pamoja na kazi nzuri wanayoifanya ya kuboresha mazingira ya utoaji wa elimu nchini kujenga pia nyumba za walimu.