
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema kuwa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima imepanua majukumu yake na sasa inatekeleza kazi kubwa zaidi ya suala la watu wazima kujua kusoma, kuandika na kuhesabu.
Akizungumza Agosti 25, 2025 jijini Dar es Salaam, Prof. Mkenda ameeleza kuwa taasisi hiyo imekuwa chachu ya mabadiliko katika elimu jumuishi na elimu bila ukomo kwa watu wote nchini.
Prof. Mkenda amefafanua kuwa mbali na kutoa maarifa ya msingi ya kuwezesha elimu kwa wananchi wote, Taasisi hiyo imejikita katika kuandaa vitabu vya kujifunzia na kufanya tafiti zinazolenga kuboresha elimu ya watu wazima na elimu bila ukomo. Tafiti hizo zimekuwa zikitumika kuunda sera na programu zinazojibu mahitaji halisi ya jamii, hususan kwa makundi yaliyo katika mazingira magumu.
Aidha, Waziri ameeleza kuwa katika kutekeleza agizo la Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Taasisi hiyo imeanzisha programu maalum ya kuwawezesha wanafunzi waliokatisha masomo kutokana na changamoto mbalimbali. Kupitia programu hiyo, zaidi ya wanafunzi 13,000 wamenufaika kwa kupata fursa ya kurejea kwenye mfumo wa elimu na kujipatia ujuzi wa maisha.
Kauli ya Prof. Mkenda inaonesha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha kila mtanzania anapata fursa ya elimu kama nyenzo ya kujenga jamii yenye uelewa, ujuzi na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.