Shule za Sekondari za Simiyu na Dodoma kufaidika na ufadhili wa dola za kimarekani milioni 10 kutoka Shirika la Maendeleo la Korea Kusini (KOICA) kwenye ujenzi wa maabara za kisasa za sayansi na TEHAMA. Mradi huo unatarajiwa kutekelezwa kwa miaka 3.

Hayo yamejiri wakati wa ziara ya Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo, na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Ndugu Atupele Mwambene nchini Korea Kusini kwa ajili ya maandalizi ya mradi huo.



Ujumbe huo ukiongozwa na Prof. Nombo umefika Ubalozi wa Tanzania jijini Seoul na kupokelewa na Balozi wa Tanzania nchini Korea, Mhe. Togolani Mavura ambapo pamoja na masuala mengine umempatia mwelekeo na muhtasari wa matokeo ya mradi huo utakapokuwa umekamilika kwa ufanisi.



Vilevile, KOICA watajenga Chuo Kikubwa cha Ufundi eneo la Kihonda mkoani Morogoro (Morogoro Polytechnic College) kitakachogharimu dola za kimarekani milioni 19.5.

Hizi ni juhudi za serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia katika kukuza na kuimarisha mafunzo ya Sayansi Teknolojia, Uhandisi na Hesabu (STEM) katika ngazi zote za elimu nchini ikiwa ni pamoja na kushirikiana na wabia wa maendeleo