
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo ameeza kuwa Serikali itaendelea kutekeleza mapinduzi ya kidigitali katika sekta ya elimu kwa kushirikiana wadau mbalimbali.
Amesema hayo Septemba 16,2025 nchini Austria wakati ujumbe wa Tanzania ulipokutana na Kampuni ya eee ya Austria.
Prof. Nombo amesema Serikali iko tayari kutumia teknolojia za TEHAMA katika ngazi zote za elimu ili kuhakikisha kunakuwa na mazingira bora ya kisasa ya ujifunzaji na ufundishaji katika ngazi zote za elimu.
Prof. Nombo amepongeza hatua ya Austria kupitia UniCredit –Bank of Austria kuendelea kufadhili Mradi wa Elimu Kidigitali unaotekelezwa Zanzibari na kueleza kuwa msaada huo utafungua fursa na kuongeza ari ya matumizi ya TEHAMA katika shule na vyuo vya Tanzania nzima.
Prof. Nombo alisisitiza kuwa ushirikiano huu ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya Elimu na Mafunzo (2014) Toleo la 2023 ambayo imeweka bayana umuhimu wa TEHAMA katika kuongeza ubora wa elimu kupitia teknolojia na ili kuandaa wahitimu wenye stadi stahiki katika soko la ajira
Kwa upande wake Bi. Theresa Wutz, Afisa Mkuu Muidhinishaji wa Miradi wa Kampuni ya eee Austria amesema wako tayari kuendeleza ushirikiano na huo na Tanzania katika kuhakikisha inafikia malengo yake katika kutumia kikamilifu Teknolojia katika mfumo wa Elimu na kukuza sayansi na Teknolojia.