Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, amepongeza Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT) kwa mchango wake katika elimu nyumbufu, akiwataka kuendelea kuzalisha wataalamu wengi wanaoweza kuajirika ndani na nje ya nchi.
Akizungumza Desemba 5, 2024, Kigoma, wakati wa Kongamano la 34 la Wanazuoni wa OUT, Prof. Nombo amesema wizara inategemea uzoefu wa OUT kufanikisha malengo ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014, Toleo la 2023, inayosisitiza elimu nyumbufu. “Tutashirikiana na OUT kuzalisha miradi yenye maendeleo kwa wananchi moja kwa moja,” amesema.
Amesema miradi kama HEET imeimarisha miundombinu, teknolojia, na kuwasaidia zaidi ya wasichana 1,000 kupata elimu ya juu.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mh. Thobias Andengenye, amepongeza OUT kwa huduma bora kwa miaka 30, akibainisha kuwa imeongeza weledi wa walimu na watendaji wa serikali za mitaa.
Mwenyekiti wa Baraza la OUT, Prof. Joseph Kuzilwa, ameishukuru wizara kwa ushirikiano, huku Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Elifas Bisanda, akieleza kuwa OUT imewasaidia Watanzania 60,000 kupata elimu ya juu.
Kongamano hilo lilifuatwa na mahafali ya 43 yaliyowahusisha wahitimu 4,307, na zoezi la upandaji miti likifanyika katika viwanja vya chuo Kigoma