Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, ametoa wito kwa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kuanzisha kozi maalum za muda mfupi na mrefu za Elimu ya Biashara.



Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Sita wa Kitaaluma wa chuo hicho uliofanyika Novemba 12, 2025 Jijini Dodoma, Prof. Nombo amesema hatua hiyo ni muhimu kwa ajili ya kuzalisha walimu wa kufundisha somo la Biashara, ambalo sasa ni la lazima kwa wanafunzi wote kwa mujibu wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014, toleo la 2023.



Prof. Nombo ameipongeza CBE kwa mafanikio ya kitaaluma, ikiwemo kushika nafasi ya nane kati ya vyuo 47 vya elimu ya juu nchini kwa mujibu wa AD Scientific Index. Alisisitiza kuwa mafanikio hayo ni kielelezo cha dhamira ya chuo katika kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita katika sekta ya viwanda na biashara.



Aidha, ameeleza kuwa CBE imefanya tafiti 418 na kuchapisha machapisho 447 ndani ya miaka mitano, akisisitiza umuhimu wa matokeo hayo kufikishwa kwa wananchi kwa lugha rahisi na inayoeleweka huku akitoa rai kwa Wizara ya Viwanda na Biashara kuendelea kutenga bajeti kwa ajili ya kuboresha miundombinu na kutoa mafunzo kwa wajasiriamali.



Amesisitiza kuwa vyuo vya elimu ya juu vina jukumu la kuhakikisha matokeo ya tafiti yanawafikia wananchi wa kawaida kwa lugha rahisi na inayoeleweka.



Ametoa rai kwa vyuo vingine nchini kuiga mfano wa CBE kwa kuandaa mikutano ya kitaaluma kama huo, kwa lengo la kubadilishana uzoefu, kuendeleza tafiti na kupanua wigo wa maarifa katika sekta mbalimbali. Ameeleza kuwa tafiti ni kiini cha mageuzi ya Taifa, na ushirikiano kati ya vyuo, Serikali na sekta binafsi ni muhimu ili kuhakikisha matokeo ya tafiti yanachochea maendeleo jumuishi.



Mkutano huo wa kitaaluma unajadili masuala muhimu yanayolenga kuimarisha ustahimilivu wa uchumi na biashara kwa maendeleo jumuishi.

Mada zilizotolewa zinahusu uchumi wa kimataifa, ujumuishaji wa kifedha, teknolojia na ubunifu, usimamizi wa mnyororo wa ugavi, soko la ajira, na siasa za kikanda na umehudhuriwa na viongozi wa serikali