Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Hussein Omar, ametoa wito kwa Watanzania gususan Vijana kutumia kikamilifu fursa ya kuwepo kwa Vituo vya Umahiri ili kupata ujuzi utakaowawezesha kubobea katika sekta muhimu za kiuchumi.



Wito huo ameutoa Agosti 7, 2025 jijini Dar es Salaam wakati wa kikao kilichowakutanisha wajumbe kutoka Jumuiya ya Vyuo Vikuu Afrika Mashariki ambao ni wasimamizi wa mradi, watekelezaji wa mradi, wawakilishi kutoka Benki ya Dunia na viongozi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.



Dkt. Omar alisema kuwa kwa sasa elimu ya ufundi stadi na mafunzo ya ufundi stadi yanatolewa kwa kuzingatia mahitaji halisi ya soko la ajira, ambapo msisitizo mkubwa umewekwa katika kuhakikisha wahitimu wanapata ujuzi wa vitendo unaowawezesha kuingia moja kwa moja katika ajira au kujiajiri.



Alieleza kuwa Vituo vya Umahiri vilivyoanzishwa kupitia Mradi wa EASTRIP vimejengwa kwa viwango vya kimataifa na vina vifaa vya kisasa vinavyowezesha utoaji wa mafunzo bora.



Alitoa rai kwa vijana na wananchi kwa ujumla kuchangamkia fursa hizo ili kujiandaa kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.



Moja wa Wajumbe kutoka Jumuiya ya Vyuo Vikuu ya Afrika Mashariki ambao ni wasimamizi wa Mradi Kikanda, Cosam Joseph ameeleza kuridhishwa na utekelezaji wa mradi huo katika nchi ya Tanzania kwa kuwa majengo yaliojengwa na vifaa vilivyowekwa ni vya kisasa ambavyo vitawawezesha wanafunzi kupata ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko la ajira la kitaifa, Kikanda na Kimataifa