Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Elimu Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt. Emmanuel Shindika amesema kupitia Mpango wa Elimu Changamani kwa Vijana Walio Nje ya Shule (IPOSA) Serikali imefanikiwa kuwarejesha katika mfumo rasmi wa elimu vijana wapatao 12,000 waliokuwa nje ya mfumo rasmi wa elimu.



Dkt. Shindika ametoa kauli hiyo katika Kilele cha Maadhimisho ya Kitaifa ya Juma la Elimu ya Watu Wazima ambapo amesema kati ya waliorejeshwa wasichana ni 6,594 na wavulana 5,406.



Ameongeza kuwa vijana hao pia wamepata ujuzi katika fani mbalimbali ikiwemo kwa kutumia programu za kompyuta ambapo baada ya kuhitimu zimewawezesha kuingia katika ajira.



Awali akizungumza kwa niaba ya Kamishna wa Elimu Mkurugenzi wa ElimuMsingi Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Maulid Mnonya amesema utaratibu kuwarejesha wanafunzi waliopata mdondoko ni hatua moja kubwa ya kupongeza Serikali kutokana na Waraka wa Elimu Namba 3 wa Mwaka 2021.



Ameongeza kuwa Sera ya Elimu ya Mwaka 2014 Toleo la 2023 imeelekeza elimu itolowe kwa watu wote, hivyo elimu ya Watu Wazima inalenga kujenga maarifa na ujuzi.



Amewataka Watanzania wote kuona fursa mbalimbali za elimu kwa walioikosa au waliopata mdondoko na kuzitumia kuwawezesha kufikia malengo yao ya elimu kupata ujuzi utakao wawezesha kushiriki katika shughuli za kiuchumi.



Nae Afisa Mafunzo kutoka Shirika la Kimataifa la DVV Bw. Matteo Mwita amesema Shirika hilo linaendelea kushirikiana na Serikali katika kuboresha mifumo ya elimu ya Watu Wazima ili kuchochea maendeleo.

0