Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe ametoa wito kwa Makatibu Tawala Wasaidizi Elimu na Maafisa Elimu wa Halmashauri Msingi kwenda kusimamia kwa weledi utekelezaji wa mitaala iliyoboreshwa ili iweze kuleta tija kwa mwanafunzi kama ilivyokusudiwa na Serikali.
Prof. Mdoe ametoa wito huo leo Januari 3, 2024 wakati akifungua Mafunzo kwa Makatibu Tawala Wasaidizi Elimu pamoja na Maafisa Elimu wa Wilaya yaliyofanyika katika ukumbi wa shule ya Msingi Bernard Bendel Kola B Morogoro.
Amesema, kama wasimamizi wa masuala ya Elimu katika ngazi ya Mkoa na Wilaya ni lazima wakasimamie vizuri utekelezaji wa mitaala hiyo iliyoboreshwa kwani tayari Wizara ya Elimu kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania imetoa mafunzo kwa Maafisa Elimu Kata na Wathibiti ubora wa elimu nchi nzima.
Amesema, Taasisi ya Elimu Tanzania itaendelea kuratibu mafunzo hayo ya utekelezaji wa mitaala iliyoboreshwa ili kuhakikisha walimu wote nchini wanapokea mafunzo hayo kupitia utaratibu wa mafunzo endelevu ya walimu kazini (MEWAKA).
Aidha, Prof. Mdoe ametoa rai kwa viongozi hao wa elimu, kufuatilia kwa undani mafunzo haya ili kufahamu namna bora ya kwenda kusimamia utekelezaji wa mtaala huo ili lengo lililokusudiwa lifikiwe bila changamoto.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) Dkt. Aneth Komba amesema mafunzo ya Mtaala ulioboreshwa kwa viongozi hao wa elimu ngazi ya mkoa na wilaya utasaidia kuongeza ufanisi na tija katika maeneo yao ya utendaji.
Ameongeza kuwa, maboresho yaliyofanyika katika mitaala hii ni pamoja na kuongeza maudhui ya kisasa, kuondoa maudhui yaliyopita na wakati na kuondoa kujirudiarudia kwa maudhui katika baadhi ya masomo, pili kupunguza wingi wa maudhui katika masomo ili kuwe na uwiano wa muda wa kujifunza, tatu maboresho katika maeneo ya ujifunzaji wa elimu ya Awali na Msingi.
Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya Maafisa Elimu Mkoa na Wilaya Afisa Elimu Mkoa wa Songwe Mwl. Michael Ligola ameishukuru Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi katika Sekta ya Elimu.