Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetangaza rasmi kuanza kwa wiki tatu za maadhimisho ya miaka 50 ya Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), yakilenga kuongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa elimu nje ya mfumo rasmi. Kauli mbiu ya maadhimisho ikiwa ni “Elimu bila ukomo kwa maendeleo endelevu.”



Uzinduzi huo umefanywa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda Julai 27, 2025 Jijini Dodoma ambapo amesema kuwa Maadhimisho hayo yataambatana na shughuli mbalimbali ikiwemo mafunzo kwa Maafisa Magereza na Wakufunzi wa elimu ya watu wa wazima na maonesho ya huduma za elimu ya watu wazima,

Aidha kutakuwa na kongamano la kitaifa litakalo wakutanisha wadau zaidi ya 1,000 kutoka ndani na nje ya nchi litakalofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.



Ameongeza kuwa Wananchi wote wanahimizwa kushiriki kikamilifu ili kujifunza, kupata ujuzi na kufurahia bunifu mbalimbali za vijana na watu wazima.

Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima ilianza rasmi mwaka 1975 na sasa imefikisha miaka 50 ikiwa na mwelekeo mpya "elimu bila ukomo" kwa watu wote ikiweka mkazo katika ujuzi pia.