Katibu Mkuu Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo anaendelea na ziara ya mafunzo nchini Afrika Kusini akiwa anaongoza timu ya wataalam kutoka Tanzania Bara na Zanzibar wanaoshughulika na Sayansi, Teknolojia na ElimuMsingi.



Ziara hiyo pia ni sehemu ya utekelezaji wa hati ya Makubaliano baina ya Tanzania na Afrika Kusini kuhusu kuhusu ElimuMsingi ikiwemo ufundishaji wa Kiswahili katika shule za Afrika Kusini.



Ujumbe huo ulipata fursa ya kutembelea shule za Msingi na Sekondari zinazotarajiwa kuwa ni shule tangulizi katika ufundishaji wa Kiswahili nchini Afrika Kusini.



Aidha, ujumbe umepata nafasi ya kutembelea Sci- Bono kituo chenye lengo la kuwahamasisha watoto kupenda masomo ya Sayansi.



Katika kituo hicho majaribio mbalimbali ya masomo ya Kemia, Fizikia na Hisabati hufundishwa kwa vitendo ikiwa na lengo la kuwawezesha watoto hao kujifunza.



Sambamba na hayo, yalifanyika majadiliano kuhusu Kiswahili kinavyofundishwa katika Chuo Kikuu cha Cape Town na Kwazulu Natal ambapo Prof. Shani Omari Mchepange na Dkt. Elizabeth Mahenge walishiriki kwa njia ya Zoom.