Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Charles Mahera, leo Disemba 20, 2024 amezindua mafunzo ya kuwajengea uwezo walimu wa Elimu ya Awali, yaliyofanyika katika Shule ya Sekondari Sokoine Memorial, mkoani Morogoro.

Mafunzo haya yanatekelezwa kupitia Programu ya BOOST kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya Rais-TAMISEMI, yakilenga kuboresha ubora wa elimu ya awali nchini.



Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Mahera alisisitiza umuhimu wa elimu ya awali kama msingi wa maendeleo ya mtoto.

“Tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa elimu ya awali ina mchango mkubwa katika maendeleo ya kiakili, kimwili, kijamii, na kihisia kwa watoto,”.



Mafunzo hayo yanalenga kuwawezesha walimu kufundisha kwa kuzingatia hatua za makuzi ya watoto kupitia mbinu bora za ufundishaji.



Zaidi ya walimu 9,000 kutoka mikoa 26 ya Tanzania Bara wanashiriki mafunzo haya ambapo mada zinazofundishwa ni pamoja na mbinu za kufundisha kupitia michezo, kutengeneza zana za kufundishia kwa kutumia rasilimali zilizopo, na kuimarisha ujifunzaji wa watoto wenye mahitaji maalum vile vile mafunzo haya pia yanalenga kuimarisha ushirikiano kati ya walimu, wazazi, na jamii katika kuboresha mazingira ya kujifunzia.



Dkt. Mahera amewashukuru wadau wa elimu, wakiwemo Benki ya Dunia, UNICEF, na USAID, kwa kushirikiana na serikali katika kuboresha elimu ya awali. Alitoa wito kwa walimu kutumia maarifa watakayopata kuleta mabadiliko chanya kwa watoto na kuhakikisha elimu ya awali inakuwa msingi thabiti wa maendeleo yao