Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Omar Juma Kipanga (Mb) amezindua zana bora za kilimo zilizotengenezwa na Kampuni ya wazawa ya IMARA TECH, Julai 01,2024 katika viwanja vya Makumbusho Kaloleni jijini Arusha.
Mhe. Kipanga amesema vijana wa Kitanzania wana nguvu kubwa ya kuchochea maendeleo katika Taifa hivyo Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi ili kuvutia makampuni mengi zaidi kuwekeza katika Teknolojia mbalimbali ambazo zinazalishwa nchini na kukidhi vigezo vya kuingia sokoni.
"Leo tumeshuhudia mfano mzuri wa tukio kubwa la utiaji saini wa mashirikiano kati ya Imara Tech na Taasisi kubwa mbili Honda na Mfuko wa dhamana kwa wakulima-PASS wakati wa uzinduzi wa zana bora za kilimo zinazozalishwa na kampuni hiyo" alisema Kipanga.
Ameongeza kuwa hadi sasa zaidi ya teknolojia 30, zilizozalishwa na wabunifu wa ndani waliowezeshwa na Serikali kupitia jukwaa la MAKISATU na kupata ufadhili kupitia COSTECH zimefikia hatua ya kuingia sokoni.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Dkt. Amos Nungu amesema Tangu kuanza kwa MAKISATU, zaidi ya Wabunifu 268 wameendelezwa kwa hatua mbalimbali, Kampuni 23 za vijana wa kitanzania zimesajiliwa tayari na zinatazamiwa kujenga viwanda na kuongeza uwepo wa bidhaa zao sokoni na zingine 47 ziko kwenye hatua za mwisho kukamilisha viwango na matakwa ya usajili wa Kampuni.
Aidha Mkurugenzi Mtendaji wa IMARA Tech Bw. Alfred Chengula ameishukuru Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia COSTECH na wadau wengine kwa kuendeleza bunifu hadi kufikia kubidhaishwa.