Serikali imetoa jumla ya shilingi bil. 310 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya shule 707 hapa nchini ukiwemo ujenzi wa shule mpya, kuongeza vyumba vya madarasa katika shule mbalimbali za sekondari zenye uhitaji pamoja na ukarabati wa miundombinu mingine ya shule hizo.



Hayo yameelezwa Julai 24, 2024 Mkoani Morogoro na Mkurugenzi wa Uthibiti Ubora wa Shule Mwl. Ephraim Simbeye wakati ufunguzi wa Mafunzo kwa Maafisa Elimu wa Mikoa, Halmashauri, Maafisa TEHAMA, Maafisa ugavi na Wakuu wa Shule za Sekondari.



Mwl Simbeye amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo Maafisa hao katika usimamizi wa miradi mbalimbali ya shule za Msingi na Sekondari

Ameongeza kuwa fedha hizo zitatumika katika kujenga madarasa mapya ya shule za Sekondari za Wavulana za Kanda, Shule za Kata, upanuzi wa Shule kwa ajili ya kidato cha Tano na ukamilishaji wa miundombinu ya Shule za Wasichana za Mikoa, hivyo amewataka Wakuu wa Shule za sekondari na Misingi kuwa wadilifu na waminifu katika kutekeleza miradi ya Serikali.



Mkurugenzi huyo amesema kupitia mradi wa Kuimarisha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) serikali imedhamiria kuboresha ufundishaji kupitia mpango wa mafunzo endelevu ya Walimu kazini (MEWAKA) ambapo Walimu wa Sayansi na Hisabati wamepatiwa mafunzo ili kuongeza umahiri wa ufundishaji darasani.