Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika kuboresha miundombinu ya Elimu kuwezesha mazingira rafiki ya ujifunzaji, kuongeza fursa za mikopo na kuzingatia maslahi bora kwa Walimu.



Rais Mwinyi amesema hayo Agosti 26, 2024 Ikulu Zanzibar wakati akizungumza katika halfa ya kuwapongeza Wanafunzi waliofaulu kwa kupata daraja la Kwanza katika Mtihani wa Kidato cha Nne 2023 na Kidato cha Sita 2024 upande wa Unguja ambapo ameeleza kuwa amefarijika kuona matokeo chanya ya uwekezaji katika sekta ya elimu.



"Natambua kuwa matokeo ya uwekezaji katika sekta ya elimu huwa hayaonekani haraka, lakini Wizara hii imefanya ya kazi nzuri na tumeanza kuona matokeo ya uwekezaji wetu mapema, hivyo nawapongeza sana" Alisema Rais Mwinyi.



Aidha Dkt. Mwinyi ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana kwa karibu sana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar katika masuala mbalimbali ya utekelezaji wa mageuzi ya Elimu.