Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, amesema kuwa mafanikio ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 yanategemea kwa kiasi kikubwa uwekezaji katika rasilimali watu, hususan kwa kutumia mfumo bora wa elimu.

Akizungumza Julai 22,2025 Jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa Mafunzo juu ya Utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 (Toleo la 2023), yaliyofanyika jijini Dodoma kwa Wamiliki wa Shule na Vyuo Visivyo vya Serikali (TAMONGSCO), Prof. Nombo alisisitiza umuhimu wa kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu mabadiliko yaliyopo kwenye sekta ya elimu.

“Ni wajibu wa Serikali kwa kushirikiana na wamiliki wa shule na vyuo visivyo vya Serikali kuhakikisha mitaala iliyopo inatumika kuandaa rasilimali watu yenye ujuzi na maarifa stahiki kwa maendeleo ya Taifa,” alisema Prof. Nombo.

Aidha, alifafanua kuwa mafunzo hayo yamelenga kuwapatia TAMONGSCO taarifa sahihi kuhusu mabadiliko ya sera, hususan katika nyanja ya Elimu Amali, ili kuwawezesha kuwekeza kwa ufanisi katika utoaji wa mafunzo hayo kwa vitendo.

“TAMONGSCO, mnapokuwa na taarifa sahihi kuhusu Elimu Amali, tuna uhakika mtaweza kufanya uwekezaji mzuri na wenye tija katika kuandaa wanafunzi wenye uwezo wa kuchangia moja kwa moja kwenye maendeleo ya uchumi wa Taifa,” amesema Katibu Mkuu.

Aidha, amewaomba TAMONGSCO kuendelea kutoa mapendekezo kuhusu Sheria ya Elimu  ambayobinafanyiwa mapitio na iko katika hatua ya wadau kutoa maoni.

Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Bw. Modest Bayo, ameipongeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kuwatambua na kuwashirikisha kikamilifu katika mchakato wa mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, Sheria ya Elimu, mabadiliko ya Mitaala pamoja na kuwapatia mafunzo juu ya mabadiliko na utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo na Mitaala iliyoboreshwa.

Aidha, alibainisha kuwa TAMNGOSTCO ilihusishwa katika zoezi la utafiti wa kitaifa, jambo linaloonyesha wazi kuwa sekta binafsi ni mshirika muhimu badala ya mpinzani.