Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Daniel Mushi, amesema wahitimu wa Chuo cha Ufundi Arusha (ATC) ni hazina kubwa kwa taifa, katika kuchochea maendeleo ya viwanda.
Prof. Mushi ameyasema hayo Disemba 05, 2024 Jijini Arusha akizungumza katika mahafali ya 16 ya Chuo hicho, ambapo zaidi ya wahitimu zaidi ya 1,000 wametunukiwa vyeti, Astashahada, Stashahada, na Shahada.
“Nawasihi kutumia vema maarifa mliyoyapata kutatua changamoto za jamii na kuchangia maendeleo ya taifa letu,” aliwaasa Prof. Mushi.
Katibu Mkuu huyo amewapongeza wahitimu kwa kufanikisha safari yao ya masomo huku akiwasihi kuwa wazalendo na waadilifu kwenye jamii zao.
Aidha amesema Serikali inajivunia uwepo wa mtambo wa kuzalisha umeme wa megawati 1.65 uliopo katika kampasi ya Kikuletwa ya Chuo hicho mkoani Kilimanjaro, ambayo sasa ni kituo cha umahiri katika nishati jadidifu.
“Hii ni hatua kubwa katika kuwajengea vijana uwezo wa kushindana kwenye soko la ajira, hasa katika sekta ya nishati ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki,” amesema Prof. Mushi.