WALIMU wa masomo ya Sayansi katika Mkoa wa Mwanza, wamepewa jukumu la kuifanya jamii kuwa ya kisayansi kwa kuhakikisha kila mtu anayepita shuleni anapata maarifa yanayoongeza thamani ya maisha yake, akielewa na kutumia sayansi katika nyanja mbalimbali za maisha.
Hayo yamesemwa Januari 16, 2024 na Afisa Elimu Mkoa wa Mwanza, Martin Mkwabi, wakati akifungua mafunzo ya siku tano kwa walimu wa sekondari wanaofundisha masomo ya Sayansi, Hisabati, na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), yanayofanyika katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Nganza, mkoani humo.
Mkwabi amesema ili kufanikisha lengo hilo, ni lazima kuwa na walimu wenye uwezo wa kufundisha na kuwavutia wanafunzi wengi kupenda masomo ya sayansi, ambao baadaye watakuwa wataalamu wa kushughulikia masuala mbalimbali kwenye jamii.
Ameongeza kuwa, licha ya changamoto za rasilimali, mwalimu mwenye ufanisi atajua jinsi ya kuchagua mbinu sahihi za ufundishaji na kutumia zana zilizopo katika eneo lake ili kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora.
Akitolea mfano kuwa hata kama vitabu vichache au vifaa vya maabara vipo, mwalimu mwenye ujuzi anaweza kutumia rasilimali kidogo zilizopo kufundisha darasa kubwa kwa ufanisi na wanafunzi wakaelewa.
Kwa upande wake Mratibu wa Mafunzo ya Kituo cha Mwanza kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Majaliwa Mkalawa, ameeleza kuwa Wizara, kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), kupitia Mradi wa Kuimarisha Ubora wa Elimu ya Sekondari nchini (SEQUIP), inaendelea kutoa mafunzo kwa walimu wa masomo ya Fizikia, Kemia, Biolojia na Hisabati pamoja na wathibiti ubora wa masomo hayo.
Amesema dhima kuu ya mafunzo hayo ni kuimarisha ubora wa elimu ya sekondari nchini kwa kuwajengea uwezo walimu, ili waweze kutumia mbinu shirikishi na kumudu mahitaji mbalimbali ya ufundishaji.