Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. James E. Mdoe amekipongeza Chuo Kikuu Mzumbe kwa utendaji bora, huku akiwataka kusimamia vizuri shughuli za maendeleo ili zikamilike kwa muda uliopangwa pamoja na kuongeza ushirikiano na Taasisi nyingine za elimu ndani na nje ya nchi.
Akizungumza na Kamati ya Menejimenti ya Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi ya Morogoro katika kikao wakati wa ziara yake iliyofanyika Septemba 4. 2023, baada ya kupokea taarifa ya maendeleo ya Chuo kutoka kwa Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha. Prof. Mdoe amesema kuwa ushirikiano ni jambo la muhimu ili kuweza kusimamia shughuli za maendeleo ya Chuo na miradi yote inayotekelezwa huku lengo hasa likiwa ni kuinua takwimu za kitaaluma kama vile kuhakikisha ongezeko la idadi ya wanafunzi kuazia ngazi za chini mpaka Uzamili ili kuleta matokeo chanya lakini pia kupanua wigo wa kufanya tafiti na kuandaa machapisho.
"Taasisi za elimu ya juu haiwezi kutofautishwa na taasisi nyingine za elimu kama haijajikita katika kufanya tafiti na kutoa machapisho, nawapongeza kwa hatua mnazozifanya katika upande huu wa tafiti na machapisho na ninawata muendelee mbele zaidi." amesema Prof. Mdoe.
Katika ziara hiyo Prof. Mdoe ametembelea miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Chuo Kikuu Mzumbe ikiwa ni pamoja na Ujenzi wa Jengo Jipya la Utawala, Jengo la Huduma za Upasuaji katika Kituo Cha Afya Chuo Kikuu Mzumbe na Ofisi za Dawati la Jinsia na Huduma Jumuishi (Mahitaji Maalumu) zinazosimamiwa na Chuo Kikuu Mzumbe,
Katika hatua nyingine, Prof. Mdoe amesisitiza juu ya utekelezaji wa mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi yaani "Higher Education for Economic Transformation - HEET Project", ambapo kwa Chuo Kikuu - Mzumbe, mradi huu unalenga kuboresha huduma za kufundishia na kujifunza, kuwajengea uwezo watumishi wa elimu ya juu ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya Teknolojia, ujenzi na uboreshaji wa miundombinu kwa Kampasi za Chuo Kikuu Mzumbe na ujenzi wa Kampasi mpya ya Chuo Kikuu Mzumbe Jijini Tanga