Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo amesema Serikali imedhamira kwa dhati ya kuendeleza elimu nchini, ikiwemo kuendelea kusimamia afua mbalimbali ili kutoa fursa za ujifunzaji kwa watu wote kupitia elimu nje ya mfumo rasmi.



Prof. Nombo amesema hayo Machi Mosi, 2024 wakati akifungua Kongamano la Kitaifa la Elimu Bila Ukomo lililofanyika jijini Dar es Salaam, linalolenga kujadili namna Bora ya kuendesha Elimu ya Watu Wazima na Elimu nje ya mfumo rasmi.



Kiongozi huyo amesema Serikali inataka kuona Elimu ya Watu Wazima inaleta mapinduzi ya kielimu, na kwa kuzingatia hilo Sera mpya ya Elimu inatoa msimamo kwamba, “Elimu nje ya mfumo rasmi itatambuliwa na watakaopitia mfumo huo watakuwa na fursa ya kujiunga na mfumo rasmi wa elimu kulingana na vigezo vitakavyowekwa”. Alisema Prof. Nombo.



Ameongeza kuwa Sera imeweka hakikisho kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, itaendelea kuimarisha na kusimamia afua mbalimbali zinazolenga kukuza fursa za elimu isiyo na ukomo kwa watu wote ili kuimarisha maendeleo endelevu ya Elimu Nchini.



Amewataka wadau mbalimbali wa maendeleo kuendelea kushirikiana na serikali pamoja na Taasisi zake ili kuleta mabadiliko endelevu katika sekta ya elimu kwa ujumla.