Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo amesema Monyesho ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yameibua fursa mbalimbali kwa Wananchi, Wadau mbalimbali wa Maendeleo pamoja na Vijana katika kujifunza teknolojia mbalimbali za kisasa.
Prof. Nombo ameeleza hayo Mei 27, 2024 jijini Tanga, wakati akitoa taarifa kuhusu Maadhimisho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu akisema ni matokeo ya uunganishwaji wa yaliyokuwa Maadhimisho ya Kitaifa ya Ubunifu na Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU), Maonesho ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi yaliyokuwa yakiratibiwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET); na Maonesho ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yaliyokuwa yakiratibiwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU).
Amesema shughuli mbalimbali zinafanyika ikiwemo ya uhamasishaji juu ya masuala elimu kwa ngazi zote ikiwa ni pamoja na elimu kwa umma kuhusu utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 toleo la mwaka 2023.
Aidha amebainisha kuwa baada ya kushindanisha Mashindano ya ujuzi katika ngazi ya Vyuo, jumla ya Wanafunzi 27 waliibuka washindi, aidha katika hatua hii ya kitaifa, watatu (3) kwa kila fani, wataandaliwa kushiriki katika mashindano ya kikanda na kimataifa yanayotarajiwa kufanyika mapema mwaka 2025.