Na Mwandishi Wetu
Timu ya Wataalamu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Ofisi ya Rais TAMISEMI pamoja na Benki ya Dunia wameshuhudia wanafunzi zaidi ya 290 wa kidato cha Kwanza wakiendelea na masomo katika shule mpya ya Msakuzi iliyojengwa katika Wilaya ya Ubungo kupitia Mradi wa Uboreshaji wa Elimu ya Sekondari (SEQUIP).
Timu hiyo imejionea hayo Machi 21, 2023 wakati walipotembelea shuleni hapo kukagua ujenzi wa miundombinu ya shule mpya ya Msakuzi iliyogharimu Shilingi milioni 470.
Shule hiyo imesaidia wanafunzi wanaoishi kwenye maeneo ya Mbezi Inn, Msakuzi na Makabe kupata shule karibu na makazi yao na kuwapunguzia adha ya kutembea umbali mrefu kufuata shule.
Wanafunzi wanaotoka katika eneo hilo walikuwa wanachaguliwa kwenda kusoma katika shule ya sekondari Mpiji Magohe ambayo ipo umbali zaidi ya kilomita 4 kutoka kwenye makazi yao.
Kwa upande wake, Mkuu wa shule ya Msakuzi amesema wanafunzi waliopangiwa kuanza kidato cha kwanza katika shule hiyo ni 290 na wote wameripoti na wanaendelea na masomo yao.
Ofisi ya Rais, TAMISEMI kupitia Mradi wa Ukuboreshaji wa Elimu ya Sekondari (SEQUIP) ilitoa Shilingi milioni 470 ya Ujenzi wa shule mpya za Kata kwa kila Halmashauri kwa ajili ya kujenga vyumba vya madarasa 8, jengo la utawala 1, maabara 3, maktaba 1, chumba cha TEHAMA 1, matundu ya vyoo 20 (wasichana 10 na wavulana 10), ununuzi wa tenki la maji 1, ujenzi wa miundombinu ya kuvuna maji na kunawa mikono.