
Katika kutekeleza mageuzi ya elimu nchini, mdahalo maalumu umefanyika ukihusisha vijana balehe waliopo nje ya mfumo rasmi wa elimu, ili kupokea maoni kuhusu aina ya ujuzi wanaopaswa kupewa ili kuwawezesha kujiajiri, kuajiri, na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi.
Akifungua mdahalo huo Jijijinj Dar es Salaam, Agosti 21, 2025, Kamishna wa Elimu, Dkt. Lyabwene Mtahabwa, amesisitiza kuwa maoni ya vijana ni nyenzo muhimu katika kufanya mapitio ya miongozo ya utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014, Toleo la 2023.
"Tunahitaji kuhakikisha kuwa elimu nje ya mfumo rasmi inatoa maarifa, maadili, na ujuzi unaoendana na muktadha wa Tanzania, kikanda na kimataifa,” amesema Dkt. Mutahaba.
Kupitia Mdahalo huo vijana wameeleza changamoto wanazokutana nazo nje ya mfumo rasmi wa elimu, ikiwemo ukosefu wa fursa za mafunzo kwa vitendo, stadi za maisha, na mbinu za kujiajiri.
UNICEF, kupitia mwakilishi wake Kiongozi wa Elimu Simone Vis ameeleza kuwa inajivunia kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na wadau wengine katika safari ya mageuzi ya elimu kutokana na miradi bunifu inayotekelezwa inayolenga kuwapa vijana hasa wasichana fursa za kujifunza, kujiamini, na kuchangia kikamilifu maendeleo katika jamii.