Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuhitimisha Kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu.



Mkenda amesema hayo Machi 09, 2024 jijini Dodoma wakati akizungumza na Waandishi wa Habari ambapo amesema Maadhimisho hayo yatafanyika Mkoani Tanga kuanzia tarehe 25 hadi 31 Mei 2024 katika Viwanja vya Michezo vya Shule ya Sekondari Popatlal.



"Maadhimisho hayo yanaongozwa na kauli inayosema _*Elimu, Ujuzi na Ubunifu kwa Uchumi Shindani*_ ambayo inachagiza umuhimu wa elimu, ujuzi na ubunifu na teknolojia katika kuchagiza maendeleo ya kiuchumi" alieleza Mkenda.



Pia amesema inaongeza hamasa ya kukuza elimu, ujuzi, na matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu kama nyenzo za kutatua changamoto za kiuchumi na kijamii.



Aidha Prof. Mkenda amesema Serikali imeendelea kuwekeza katika kuendeleza na kubiasharisha bunifu na teknolojia zinazobuniwa Nchini na kwamba katika kipindi cha mwaka 2019 na 2023 zaidi ya bunifu *2,000* zimetambuliwa na kati ya hizo bunifu *283* zinaendelezwa na Bunifu *42* zimeweza kufikia hatua ya kubiasharishwa na ziko sokoni.



Matukio yatakayohusika katika Maadhimisho hayo ni pamoja na Maonesho ya bidhaa, bunifu na teknolojia;
Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU); Mashindano ya ujuzi *'Skills Competition*' kwa Wanafunzi wa Vyuo vya Ufundi na Ufundi Stadi; Mikutano na Midahalo na Mafunzo kwa wabunifu