Tanzania imefanya mageuzi katika mitaala ambayo ni utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuwa na mitaala inayojikita katika ujuzi.



Hayo yamesemwa na Prof. Carolyne Nombo Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Julai 17, 2024 alipotembelea na kukutana na uongozi wa Chuo cha Ufundi cha Tshwane South nchini Afrika Kusini.



Aidha, ameeleza kuwa Tanzania iko katika hatua ya kuandaa mkakati wa Ugharamiaji wa Uendelezaji wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (TVET Financing Strategy) na ziara hiyo ni katika kuendelea kujifunza mifumo mbalimbali ya nchi juu ya utekelezaji wa mafunzo ya ufundi.



Prof. Nombo ameeleza kuwa ziara hii imekuwa ni fursa nzuri ya kujifunza jinsi Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (TVET) inavyogharamiwa.



Katika ziara hiyo chuoni hapo Katibu Mkuu ameambatana na Mkurugenzi wa Elimu ya Ufundi, Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Elimu Msingi.



Afrika Kusini ina jumla ya vyuo vya TVET 50 na kampasi 280 huku uelekeo wa mafunzo ya ufundi nchini humo ni vigezo vya Utengenezaji na Uboreshaji wa Mitaala. (Occupational Standards).