Dr. Charles Msonde, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI (ELIMU), ameanza rasmi ziara yake ya kikazi Mkoa wa Dodoma Leo Mei 27, 2024 kwa kuzungumza na Walimu wa shule za Msingi na Sekondari za Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwenye ukumbi wa Shule ya Msingi St. Gasper iliyopo Miyuji.
Katika kikao hicho, Dr. Msonde ametatua changamoto mbalimbali zinazowakabili walimu kwa ujumla ikiwa ni pamoja na upandishwaji wa madaraja, madai ya malipo, likizo, uhamisho, maslahi n.k
"Nchi yetu ilianza rasmi safari ya mabadiliko ya kuboresha Elimu nchini mnamo Januari 2021 na safari hiyo imefanikiwa kutatua changamoto kadhaa zinazowakabili walimu nchini. Serikali imeamua kuhakikisha kero zote za walimu zinaisha kwa kuwa viongozi wa awamu ya Sita wanawapenda walimu.
"Katika kipindi hiki, madaraja ya Walimu yanapitiwa upya na takribani walimu 54,000 watapandishwa madaraja ya mserereko. Pia tumeshughulikia masuala ya madai ya malipo kwa ajili ya likizo, hamisho pamoja na maslahi. Watumishi wa Serikali wawe na lugha nzuri wanapowahudumia walimu pindi wanapokua na changamoto" Amesisitiza Dr. Msonde.
Awali akiongea kama mwenyeji, Katibu Tawala Msaidizi seksheni ya Elimu Mkoa wa Dodoma Mwl. Vicent Kayombo, ameeleza mikakati mbalimbali iliyowekwa na Mkoa katika kunyanyua Taaluma ikiwemo ufaulu ikiwa ni pamoja na Mkakati wa Elimu 2024 unayosema "Uwajibikaji wangu ndio msingi wa kuinua ubora wa Elimu na ufaulu Dodoma".
Kadhalika, Mwl. Kayombo amesema Mkoa umefanikiwa kuandaa mafunzo kwa wenyeviti wa bodi na kamati za shule za Msingi na Sekondari ambayo bado yanaendelea Mkoa hapo ambapo mpaka Sasa, wenyeviti 800 wameshapatiwa mafunzo hayo. Pia Mkoa umeunda jopo la ufuatiliaji utekelezaji wa majukumu ya Walimu ambapo shule 180 zilifikiwa.
Ziara ya Naibu Katibu Mkuu huyo ambayo ni ya siku 6 kwa Halmashauri za Mkoa wa Dodoma, imekuja kipindi muafaka cha utekelezaji wa Mkakati wa Elimu wa Mkoa kwani inalenga kuzungumza na Walimu juu ya kero na changamoto zinazowakabili katika utekelezaji wa majukumu yao ukizingatia kada hiyo ni muhimili muhimu kwenye jamii na Taifa kwa ujumla.